Shirika lisilo la Kiserikali la Caring Hearts (CAHE) tulialikwa na kushiriki katika Uzinduzi wa Wodi la Akina Mama katika Zahanati ya Ipalamwa Mwezi Machiambayo ipo chini ya Usimamizi wa Shirika la Global Volunteers lenye Makao yake Makuu nchini Marekani.
Mkurugenzi wa shirika la Global Volunteer nchini Tanzania Bw. Nayman Chavalla amesema, jengo hilo ambalo lina thamani ya zaidi ya Tshs. 194,000,000/= limefadhiliwa na Familia ya Peter J. King kutoka Marekani.
Naye Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ipalamwa Dkt. Silas Mosha amesema, kupitia Wodi hilo Akina Mama watanufaika na huduma za afya, mafunzo ya lishe kwa ajili ya akina mama hao kujiandaa kujifungua pamoja na wasioweza kujifungua kwa njia ya kawaida.
Dkt. Mosha amesema, wapo akina mama wasioweza kujifungua kwa njia ya kawaida hivyo wakijulikana mapema wanaweza kupata huduma ya afya inayohitajika kwa lengo la kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa kujifungua.
Uzinduzi huo ambao ulifanywa na Askofu Mstaafu wa Dayosisi ya Iringa Prof. O.M. Mdegella ulihudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.


 
  
  
  
  
  
  
 